Samaki Na Dagaa Wanasaidia Kupunguza Uzito Mkubwa Na Kitambi

Samaki na Dagaa Wanafaa Kwenye Safari ya Kupunguza Uzito?

Ili kuwa na Uzito unaotakiwa bila kuwa na kitambi ni muhimu uwe na elimu pana kuhusu chakula.

Ninakiri kwamba kuna mitazamo mtambuka kuhusiana na mada hii Kutoka na tafsiri ya elimu na tafiti zilizopo kuhusu mada husika na pia uzoefu binafsi.

Katika somo hili nimekueleza na kukushauri kulingana na tafiti zinazoaminika zinachosema kuhusiana na samaki na dagaa ikiwa wanafaa kwenye safari ya kupunguza uzito na kitambi.

Ni sawa ikiwa hadi mwisho utabaki kuwa na mtazamo tofuati na mimi…”

Siku zote tunapaswa kuchagua kufanya au kutofanya kitu kwa kulinganisha faida na hasara zake. Kama faida ni kubwa kuliko hasara basi tunafanya. Ikiwa hasara ni nyingi licha ya kuwa na faida kidogo tunaacha!

Binafsi huwa nakula Samaki na dagaa.. hata hivyo soma hadi mwisho nitakupatia ushauri kulingana na yote ninayofahamu kuhusiana na hili.

Tuanze kwa kuangazia faida za kula Samaki na dagaa  katika mlengo wa kuchoma mafuta na kuboresha afya..

Faida Za Kula Samaki

  1. Mafuta ya Omega 3

Hii ni faida ya kwanza na kubwa zaidi ya kula samaki. Mafuta ya omega 3 fatty acids ni aina ya mafuta muhimu ambayo yanasaidia kwenye afya ya ubongo.

Kwenye samaki yanapatikana katika namna ambayo tayari yametengeneka tofuati na mafuta ya omega 3 kutoka kwenye mimea ambayo unayapata kama malighafi na mwili utayatumia kutengeneza omega 3 inayohitaji.

  1. Virutubisho

Kwenye samaki unapata virutubisho vingine kama protini, vitamin, madini kama madini ya chuma, magnesium, zinc, madini joto ‘iodine’, kalsium na potassium.

Hasara Za Kula Samaki na Dagaa

Hasara za samaki na dagaa kwenye kupunguza Uzito na kitambi zinatokana ukweli kwamba haviwezi kusaidia kwenye vyanzo vya tatizo ambalo ni

“.. Usugu wa insulin na mioto (inflammation)..’’

Sio samaki wala mafuta yake yanaweza kusaidia katika maeneo hayo ambayo ndio yanafanya uwe na uzito mkubwa au kitambi.

  1. Inapandisha Insulin na Usugu wa Insulin

Kila unapokula Samaki au dagaa insulin inapanda kwa kiasi cha kutosha.. usidhani inapanda unapokula tu sukari..

Chukulia mfano wa masikio ya kawaida. Mtu akiwa muda mwingi yupo kwenye makelele makubwa, uwezo wa masikio unapungua. Itafika hatua hasikii sauti za kawaida. Ili asikie anahitaji sauti kubwa sana ambayo kwa watu wa kawaida ni kelele.

Inatokea hivyo hata kwa mtu ambaye amezoa kuwa na kiwango kukubwa sana cha insulin kwenye mwili wake muda mwingi. Na hivi vinatengeneza usugu wa insulin. Asilimia kubwa ni kwa sababu ya chakula tunachokula na wachache wanazaliwa na changamoto hii.

Kwahiyo kama njia mojawapo ya kupambana na usugu wa insulin ni kudhibiti vyakula vinavyopandisha kwa kiasi kikubwa insulin kwenye damu. Karibu kila chakula kinapandisha insulin, lakini vinatofuatiana kiwango.

Ni muhimu kuvifaham na kupunguza vile vinavyopandisha kwa kiasi kikubwa. Ukifanya hivyo wakati ukiwa na uzito mkubwa na kitambi, inamaana itakusaidia upungue haraka.

Mara nyingi imekuwa inapozungumziwa suala la vyakula vinavyopandisha insulin kwenye damu vimekuwa vinazungumziwa vyakula vya wanga na sukari. Lakini insulin inahusika na vyakula vya protini na mafuta pia. Wanaolaumu wanga na sukari kuwa ndio vinaongeza kiwango cha wanga wanakusukuma kula nyama na mafuta kwa wingi.

Lakini tazama! Protini pure, mafuta pure na sukari pure vyote vinapandisha insulin katika kiwango sawa sawa.[1] Yaani mtu aliyekula nyama ya ng’ombe, aliyekunywa mafuta na aliyekula sukari wote lao moja, insulin inapanda. Sio tu nyama ya ng’ombe hata samaki, maziwa, mayai pia.

Namna hatari zaidi kwenye mlo unayoweza kufanya ni kuchanganya protini ya wanyama na chakula cha wanga.[2] Insulin inapanda sana ni kama vile umekula sukari yenyewe tu. Haya sasa ndugu yangu mpenzi wa ugali samaki, wali nyama, ndizi nyama na ndugu zake hili linakuhusu. Ukiendelea na aina hii ya milo hakuna dawa ya kitambi itakusaidia. Kwa sababu usugu wa insulini hautaondoka.

Ona huu mfano…

Ukila viazi vitamu umeponda ponda pamoja na samaki (protini ya wanyama), insulin inapanda kwa asilimia 50 zaidi kuliko ungekula viazi peke yake.[3] Lakini badala ya samaki ukaweka brokoli (protini ya mimea) kupanda kwa insulin kunashuka kwa asimilia 40% zaidi kuliko ungekula viazi vitamu peke yake.[4]

  1. Haisaidii Kupunguza Uzito

Mafuta ya samaki yanasifika sana kwa sababu ya wingi wa mafuta ya omega 3. Ambayo yanasaidia kuzima mioto. Lakini sayansi haioneshi hivyo. Watu walipewa mafuta ya samaki kiasi sawa na kula Samaki wenye mafuta ya kutosha kama tuna, salmon nk. Haikuwasaidia katika kupunguza mioto (inflammation)[5] wala kupunguza uzito.[6]

  1. Sumu na kemikali za baharini

Uwezo wa Samaki kutunza sumu na kemikali zilizopo kwenye mazingira wanayoishi unapunguza thamani ya virutubisho vinavyopatikana kwa kula samaki. Hii ni kutokana na sumu na kemikali zinazoyeyuka kwenye mafuta (fat-soluble pollutants) ambazo zinalundikana kwenye miili ya viumbe vya baharini.

Kumbuka dunia tuliyonayo leo sio ile ya watu elfu tano kula samaki wawili na mikate mitano..

Mfano wa hizi kemikali ni;

Organotins

Hizi ni kemikali rangi zilizokuwa zinapakwa kwevye vyombo vya baharini kama meli na boti kabla ya kupigwa marufuku mwaka 2008[7] kwa sababu..

  1. Zilikuwa zinavuruga mfumo wa homoni wa viumbe, kiasi kwamba ziliwafanya konokono wa kike kuota uume[8]
  2. Inahamasisha peroxisome proliferator-activated receptor gamma (PPAR-γ) ambayo huyu ni mkuu wa kutengeneza seli mpya za mafuta na kuhamasisha mwili kutunza mafuta zaidi.

Organotins kwa binadamu zinasababisha kuongezeka kwa idadi ya seli za mafuta za kudumu[9] (hata kwa watu wazima) na seli za mafuta kutanuka.

Pamoja na kwamba organotins zilizuiliwa miaka mingi imepita lakini bado hizi kemikali zipo kwenye maji na kiwango chake kinachoonekana kwenye samaki na vyakula vingine vya baharini ni sawa na ilivyokuwa kabla ya katazo.[10]

Hata hivyo inaonekana kuwa samaki waliopatikana kibiashara wanakuwa na kiwango kikubwa zaidi cha organitins kuliko waliovuliwa kienyeji.[11] Na pia hakuna bado taarifa za kiutafiti kujua kiwango cha hizi kemikali kwenye maji ya ziwa na bahari ya nchi yetu Tanzania.

Bisphenol A (BPA)

BPA (bisphenol A) iligunduliwa zaidi ya karne iliyopita kama estrogen ya kutengeneza.

Estrogen imezoeleka kitaa kama ‘homoni ya kike’ ni homoni ambayo ipo kwa wanaume na wanawake; ipo kwa wingi kwa wanawake kuliko wanaume.

Mwanaume akiwa na homoni hii kwa wingi, anapoteza uanaume wake..

Yaani..

Zile sifa za kiume kama urijali zinapungua, mwanaume utajikuta zile nguvu zingine zimepungua.

Lakini pia..

Estrogen ni homoni ambayo inahamasisha mwili kutunza mafuta zaidi. Ikiongezeka inaongezeka pamoja na homoni zingine kama insulin, inapelekea mwili kuongezeka uzito na kitambi.

Vyanzo vya BPA

Kwa sehemu kubwa BPA (zaidi ya 90%) inapatikana kwenye chakula.. ndio maana ukifunga kwa siku chache kiwango cha BPA kwenye mwili wako kinapungua.[12]

Vyakula Gani?

  • Vya makopo au vilivyofungashwa kwenye packets. Ukiviepuka kwa siku tatu unapunguza BPA mwilini kwa 76%[13].
  • Vyakula vya baharini kama Samaki wanakuwa na kiwango kikubwa cha BPA kutokana na uchafuzi wa bahari na maziwa uliokithiri kwa sasa. Wakati mwingine hawa samaki wanaweza wakawa na kiasi kikubwa cha BPA kuliko hata samaki wa kopo.[14]
  1. Havina Nyuzilishe

Nyuzilishe zinapatikana kwenye MIMEA TU![15]

Hakuna nyuzilishe hata moja kwenye nyama, samaki, mayai wala maziwa. Kila mtu anatakiwa kupata kuanzia gram 30 za nyuzlishe kwa siku.[16]

Kwa kawaida ukila vyakula ambavyo vinatokana na mimea katika uasili wake unapata zaidi ya nyuzilishe unazohitaji kwa siku. Hata hivyo kutoka na wazazi wetu wa kale, inaonekana miili yetu ilitengenezwa kupata angalau gram 100 za nyuzilishe kwa siku.[17]

Ukila chakula chenye kalori nyingi bila nyuzilishe, utaishia kunenepa kwa sababu hamu ya kula itazidi kuwa kubwa kila wakati. Licha ya kuwa na kalori nyingi hakuna kitu kinachousaidia mwili kujua upunguze hamu ya kula.

Matunda, mbogamboga, nafaka nzima na jamii ya maharage ndio chanzo cha nyuzilishe. Kwa kula Samaki na dagaa kwa wingi unakosa nyuzilishe na hivyo huwezi kuchoma mafuta.

Ushauri Wangu

  1. Ukiwa kwenye hatua ya kwanza yaani bado unapambana na uzito mkubwa au kitambi au unataka kutibu ugonjwa mwingine unaohusiana na usugu wa insulin kama
  • Kisukari
  • Presha
  • Saratani Nk

Ni vema ukaacha kabisa matumizi ya Samaki na dagaa aina zote hadi utakapofikia lengo lako.

  1. Ukishafikia lengo lako katika maisha yako ya kawaida unaweza ukala samaki kwa kiasi kidogo na kula chakula hai kwa kiasi kikubwa. Ukizingatia Samaki na dagaa ni chakula chenye ubora mdogo katika ulimwengu wa leo.
  2. Ukitaka kula Samaki au dagaa zingatia haya
    1. Asikaangwe kwenye mafuta! Anatakiwa akiwa mbichi, aliyekaushwa au kuchomwa lakini sio kukaangwa kwa kutumbukizwa kwenye mafuta
    2. Samaki na dagaa bora ni wale wanaopatikana kwenye maji yasiyo na shughuli za binadamu ‘wild caught’ ambapo hakuna sumu za bahari au madawa ya kufugia
    3. Kwa matokeo bora usichanganye samaki au dagaa na chakula cha wanga kama viazi, wali, ugali.
    4. Chagua samaki ambao wana mapezi na magamba kwa sababu hawatunzi sana kemikali za baharini na pia waliruhusiwa na Mwenyezi Mungu kutumika kama chakula katika viumbe wa baharini (Mambo Ya Walawi 11:9-12).

REJEA:

[1] Nuttall FQ, Mooradian AD, Gannon MC, Billington C, Krezowski P. Effect of protein ingestion on the glucose and insulin response to a standardized oral glucose load. Diabetes Care. 1984;7(5):465–70.

[2] Sun L, Ranawana DV, Leow MK, Henry CJ. Effect of chicken, fat and vegetable on glycaemia and insulinaemia to a white rice-based meal in healthy adults. Eur J Nutr. 2014;53(8):1719–26.

[3] Gulliford MC, Bicknell EJ, Scarpello JH. Differential effect of protein and fat ingestion on blood glucose responses to high-and low-glycemic-index carbohydrates in noninsulin-dependent diabetic subjects. Am J Clin Nutr. 1989;50(4):773–7.

[4] Ballance S, Knutsen SH, Fosvold ØW, Wickham M, Trenado CD, Monro J. Glyceamic and insulinaemic response to mashed potato alone, or with broccoli, broccoli fibre or cellulose in healthy adults. Eur J Nutr. 2018;57(1):199–207.

[5] Buoite Stella A, Gortan Cappellari G, Barazzoni R, Zanetti M. Update on the impact of omega 3 fatty acids on inflammation, insulin resistance and sarcopenia: a review. Int J Mol Sci. 2018;19(1):218.

[6] Du S, Jin J, Fang W, Su Q. Does fish oil have an anti-obesity effect in overweight/obese adults? A meta-analysis of randomized controlled trials. PLoS ONE. 2015;10(11):e0142652.

[7] Filipkowska A, Złoch I, Wawrzyniak-Wydrowska B, Kowalewska G. Organotins in fish muscle and liver from the Polish coast of the Baltic Sea: is the total ban successful? Mar Pollut Bull. 2016;111(1–2):493–9.

[8] Sousa ACA, Pastorinho MR, Takahashi S, et al. History on organotin compounds, from snails to humans. Environ Chem Lett. 2014:12(117);117–37.

[9] Janesick AS, Blumberg B. Obesogens: an emerging threat to public health. Am J Obstet Gynecol. 2016;214(5):559– 65.

[10] Filipkowska A, Złoch I, Wawrzyniak-Wydrowska B, Kowalewska G. Organotins in fish muscle and liver from the Polish coast of the Baltic Sea: is the total ban successful? Mar Pollut Bull. 2016;111(1–2):493–9.

[11]  Cardwell RD, Keithly J, Simmonds J. Tributyltin in U.S. market-bought seafood and assessment of human health risks. Hum Ecol Risk Assess. 1999;5(2):317–35.

[12] Christensen KL, Lorber M, Koslitz S, Brüning T, Koch HM. The contribution of diet to total bisphenol A body burden in humans: results of a 48 hour fasting study. Environ Int. 2012;50:7–14.

[13] Rudel RA, Gray JM, Engel CL, et al. Food packaging and bisphenol A and bis(2-ethyhexyl) phthalate exposure: findings from a dietary intervention. Environ Health Perspect. 2011;119(7):914–20.

[14] Repossi A, Farabegoli F, Gazzotti T, Zironi E, Pagliuca G. Bisphenol A in edible part of seafood. Ital J Food Saf. 2016;5(2):5666.

[15] Institute of Medicine (U.S.). Dietary Reference Intakes: Proposed Definition of Dietary Fiber. Washington, D.C.: National Academies Press; 2001.

[16] Institute of Medicine. Dietary Reference Intakes for Energy, Carbohydrate, Fiber, Fat, Fatty Acids, Cholesterol, Protein and Amino Acids. Washington, D.C.: National Academies Press; 2005.

[17] Jew S, Abumweis SS, Jones PJ. Evolution of the human diet: linking our ancestral diet to modern functional foods as a means of chronic disease prevention. J Med Food. 2009;12(5):925–34.

0 0 votes
Article Rating
Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Share
Scroll to Top