Aina ya SUMU Zinazoongeza Uzito & Kitambi

Aina ya SUMU Zinazoongeza Uzito & Kitambi

Unataka kupunguza uzito au kitambi? Fanya ‘detox‘ wakimaanisha ‘toa sumu’.

Wanafanya hivyo wakifahamu kuwa hadi mtu unakuwa na uzito mkubwa na kitambi ni kwa sababu ya SUMU nyingi ambazo zimelundikana mwilini.

Ili upungue itakubidi utoe kwanza sumu mwilini. Kuna bidhaa nyingi sana za kufanya detox, huenda hata wewe umewahi kutumia.

Kuna dawa/bidhaa zingine ni balaa.. Ukitumia utaharisha na kutapika nusu kufa..!

Mama mmoja alitaka kumfungulia kesi mtaalamu wa tiba asili aliyemuuzia dawa ya kupunguza uzito, ilimfanya akaharisha na kutapika akawa hoi. Alilazwa hospitali ya mkoa wa Morogoro siku 2.

Kwa maelezo ya mtaalam; ukiharisha na kutapika ndio unaondoa sumu zinazokufanya uonekane mnene.

Lakini…

Hata kama kweli kuna sumu zinazokufanya unenepeane; je, zimelundikana kwenye mfumo wa chakula kwamba unaweza ukazitoa kwa kuharisha?

Sumu ni nini?

Sumu ni kemikali au molekyuli inayowezakuwa na madhara kwa afya ya binadamu, wanyama, au mazingira.

Sumu inaweza kuwa katika aina tofauti, kama vile kemikali, gesi, madini tembo ‘heavy metals’, mazao yanayotokana na shughuli za kibaolojia za mwili, au hata sumu za asili kutoka kwa mimea au wanyama.

Athari za sumu kwa mwili zinaweza kutofautiana kutoka kwa madhara madogo kama mzio au kuumwa kidogo hadi madhara makubwa kama kuvuruga mifumo wa mwili kama mfumo wa homoni, neva na damu, uharibifu wa viungo au hata kifo.

Madhara ya sumu yanategemea aina ya sumu, kipimo kilichopokelewa, njia ya kuingia mwilini (kama vile kupitia ngozi, kuvuta pumzi au kumeza), na muda wa ambao sumu imeingiliana na seli za mwili.

Sumu hutumiwa pia kwa makusudi katika maeneo kama vile maabara ya kisayansi, kwa mfano, kwa madhumuni ya utafiti au katika utengenezaji wa dawa.

Inawezekana sumu zikamfanya mtu kuongezeka uzito?

Mojawapo ya mifumo ya mwili inayoweza kuathiriwa na sumu ni mfumo wa homoni ‘endocrine system’. Huu mfumo kwa sehemu kubwa sana unahusika katika uzito na kitambi.

Sumu haziongezi uzito moja kwa moja, ila zinaleta madhara kwa kubadilisha mfumo wa homoni na hivyo uzito na kitambi vinakuja kama matokeo ya uharibifu huo.

Hata hivyo..

Sio sumu zote ambazo zinaathiri mfumo wa homoni na kupelekea kuongezeka. Hapa chini nitakueleza zile ambazo zinahusika.

Sumu ambazo zinasababisha uongezeke uzito au kitambi

Dawa

Dawa zote huwa zinakuwa na madhara ambayo hayajakusudiwa ‘side effects’. Baadhi ya dawa hayo madhara yanathiri mfumo wa homoni na kumfanya mtu kuhifadhi mafuta mengi. Dawa hizo ni:

Dawa za kisukari

Nyingi kati ya hizi kuanzia zile za kumeza kama glyburide, glipizide, rosiglitazone, pioglitazone hadi zile za kuchoma ‘insulin’ zinasababisha mtu kuongeza uzito.

Dawa za sonona ‘antidepressants’

Baadhi ya dawa za kupambana na msongo wa mawazo zinavuruga mfumo w a mawasiliano wa mwili sehemu ya kutawala hamu ya kula na kupelekea mtu kuongezeka uzito.

Hizi ni zile ambazo zipo kwenye kundi la tricyclic antidepressants na selective serotonin reuptake inhibitors (SSRIs) kama vile Amitriptyline, Fluoxetine, Paroxetine, Sertraline na Mirtazapine.

Dawa za magonjwa ya akili ‘antipsychotics’

Dawa zingine zinazotumika kwa magonjwa ya akili kama olanzapine and clozapine Olanzapine, Risperidone, Quetiapine na Aripiprazole zinavuruga mfumo wa homoni na kuongeza hamu ya kula. Matokeo yake ni kuongezeka uzito.

Steroids

Dawa za aina hii ni kama prednisone na sindano na vidonge vya uzazi wa mpango. Pamoja na vipandikizi vinavyotumika kwenye uzazi wa mpango.

Hili ni kundi ambalo wengi hasa wanawake huwa wanalishau kwamba linaweza kusababisha wakawa na uzito mkubwa na kitambi ukiachana na chips soda..!

Mama hajambo tu ‘miss’ miezi michache baada ya sindano, vidonge au kipandikizi kiuno hakionekani. Hata ‘P2’ nazo ni dawa za steroids.

Organotins

Ni aina ya kemikali ambayo ilikuwa inapakwa kwenye vyombo vya baharini, mabomba makubwa ya mafuta na vifaa kama ‘cage’ za kufugia samaki ili kuzuia mimea ya majini kama magugu maji isishikane.

Baadaye iligundulika kwamba konokono wa kike waliokuwa katika maeneo yale waliota ‘uume’. Hii ikwavutia wengi kufanya utafiti.

Ikaonekana hizi kemikali zinavuruga mfumo wa homoni na ni hatari sio tu kwa viumbe wa majini lakini pia wanadamu wanaotumia viumbe hao kama chakula.

Pamoja na kwamba kemikali hizi zilipigwa marufuku duniani kote mwaka 2008 kutumika kwenye vifaa vya majini lakini kiwango cha mabaki ya kemikali hizo kwa viumbe wa majini kipo sawa leo sawa na ilivyokuwa kabla ya katazo.

Kwani inafanyaje?

Organotoxin inahamasisha peroxisome proliferator-activated receptor gamma (PPAR-γ) ambayo ni bingwa wa kutengeneza seli mpya za mafuta mwilini.

Kwa kawaida mtu anatengeneza seli za mafuta utotoni. Akiwa mtu mzima seli za mafuta haziongezeki ila zinaongezeka ukubwa.

Ukiona mtu mzima alikuwa kawaida amenenepa mara nyingi inakuwa kwa sababu seli za mafuta zimeongezeka ukubwa na sio idadi.

Hizi sumu zinapohamasisha PPAR-γ zinahamasisha mwili kutengeneza seli mpya za mafuta hata kwa watu wazima.

Seli hizi mpya zinatengenezwa kutoka kwenye selishina za mwili hasa za kwenye mifupa. Selishina ni seli ambazo hazijakomaa kwahiyo zinaweza kutengeneza seli za aina nyingine.

Matumizi ya selishina hizokutengeneza seli za mafuta ni hasara kwa mwili kwa sababu viungo vingine kama mifupa inakosa seli za kuijenga na utakuta mtu anashida ya kuwa a mafuta mengi mwilini ‘uzito au kitambi’ pamoja na shida ya mifupa isiyoimara ‘osteoporosis‘.

Inatokea hivyo hivyo kwa wagonjwa wanatumia dawa ya kisukari inayoitwa ‘rosiglitazone‘.

Aina hii ya kuongezeka uzito ni ngumu sana kupunguza uzito. Sio kwamba haiwezekani, ila utahitaji jitihada kubwa zaidi na uvumilivu mwingi hadi ufikie lengo.

Imeonekana kuwa unapokula samaki walitoka kwenye maeno haya wanakuwa na kiwango fulani cha hizi kemikali. Hata hivyo kiwango cha sumu hizi kinatofuatiana kati ya aina ya samaki na maeneo duniani.

Samaki wenye kiwango kikubwa cha organotins ni tuna fish, halibut fish na sword fish.

Nikiwaangalia hawa samaki naona wanasifa zinakaribia kufanana. Kabla sijafanya hitimisho nakumbuka kile Mungu ‘aliyewaumba hawa viumbe’ alichosema

Na hao wote wasio na mapezi na magamba, ndani ya bahari, na ndani ya mito, katika hao waendao majini, na kayika wote wenye uhai, waliomo majini, haoni machukizo kwenu.

Mambo ya Walawi 11:10, SUV

Utagundua hao samaki wote hawana magamba ‘scales’ japo wana mapezi. Inaonekana samaki wenye mapezi na magamba kama sato wanauwezo mkubwa wa kujilinda au kuharibu sumu mbalimbali na hivyo kutulinda sisi.

Lakini pia inawezekana kuna zaidi ya hapo. Kinachoweza kutusaidia ni kubakia kwenye kile ambacho tumefunuliwa katika tafiti za kisayansi na neno la Mungu.

Ushauri Wangu

 1. Punguza matumizi matumizi ya vyakula vya baharini kama samaki na dagaa. Ongeza mbadala wake kama flaxseeds ili kupata mafuta ya omega 3 ya kutosha bila madhara.
 2. Ikiwa unataka kutumia wanyama wa baharini hakikisha wanasifa mbili: wanamapezi na magamba. Kama hawana hizo sifa achana nao.
 3. Kama unaweza kupata samaki wanaopatikana kwenye maji yasiyo na shughuli nyingi za binadamu zenye kutumia kemikali unaweza ukawatumia bila kuwa na mashaka. Lakini kwa hawa samaki wanaopatikana kibiashara zaidi kuwa nao makini hadi itakapothibitishwa vinginevyo.

Hii ni mojwapo ya sababu kwanini kwenye program yangu ya ‘Permanent Weightloss’ Nashauri upunguze au kuepuka matumizi ya samaki pia.

Plastiki

Unakumbuka bara linaitwa ‘arctic’ lipo mbali huko kwenye baridi hawaishi watu, lakini ilionekana huko pia kuna vipande vya plastiki vimepelekwa na bahari.

Plastiki kwa sasa ni tatizo, zimejaa kila mahali… unakumbuka hata Tanzania walizuia mifuko ya plastiki kipindi kile?

Sio tu kwamba plastiki haziozi zinaharibu mazingira lakini pia zina madhara kwa afya ya binadamu. Zipo aina nyingi za plastiki, hapa nitazungumzia zile tu zinazoathiri uzito.

Bisphenol A (BPA)

BPA (bisphenol A) iligunduliwa zaidi ya karne iliyopita kama estrogen ya kutengeneza.

Estrogen imezoeleka kitaa kama ‘homoni ya kike’ ni homoni ambayo ipo kwa wanaume na wanawake; lakini ipo kwa wingi zaidi kwa wanawake kuliko wanaume.

Mwanaume akiwa na homoni hii kwa wingi, anapoteza uanaume wake..

Yaani..

Zile sifa za kiume kama urijali zinapungua, mwanaume utajikuta zile nguvu zingine zimepungua.

Lakini pia..

Estrogen ni homoni ambayo inahamasisha mwili kutunza mafuta zaidi. Ikiongezeka inaongezeka pamoja na homoni zingine kama insulin, inapelekea mwili kuongezeka uzito na kitambi.

Hadi miaka ya 1950 ilionekana kwamba inaweza kutumika kutengeneza aina ya plastiki inayoitwa polycarbonate.

Pamoja na kwamba walifahamu madhara ya hii kemikali iliendelea kutumika na kusambazwa dunia nzima. Hadi leo takribani puound bilioni 6 zinazalishwa kila mwaka.

Vyanzo vya BPA

Pamoja na kwamba plastiki za polycarbonate zinatumika kutengeneza vifaa na vitu vingi ambavyo tunavitumia kila siku bado sio kila kilichotengenezwa kwa polycarbonate kinaleta madhara kwa binadamu.

 • Polycarbonate inatumika kutengeneza vioo vya usalama kama vya kwenye majengo makubwa, stendi za mabus, viwanja vya ndege, vioo vya magari na ndege, nk
 • Vyombo vya kuhifadhia chakula kama mabakuli
 • Vifuniko vya kutunzia vifaa kama kamera, mashine za kiwandani na vifaa vya umeme
 • Chupa za kuhifadhia maji

Polycarbonate ina matumizi mengi mengi sana ambayo ni mazuri..

“SIO KILA” kifaa kilichotengenezwa kwa polycarbonate kitakudhuru

Ila ‘CHAKULA’ kinaoongoza kwa 90%..

Kuchangia kiasi cha BPA ambacho mwanadamu anakipata kwenye mwili wake.

Nikupe ushahidi..

‘Ukifunga kwa siku chache kiwango cha BPA kinapungua kwenye mwili mara kumi.’

Hii inatokea sio kwa sababu umejiepusha na mazingira yenye vifaa vilivyotengenezwa kwa hizo plastiki ila kwa sababu hajala

Inaonekana hizi kemikali kwa wingi tunazipata kwenye chakula.

Hata hivyo huhitaji kufunga siku nyingi ili upate faida hii, unaweza ukapunguza kiwango cha BPA kwenye mwili wako kwa asilimia 76% kwa kuepuka vyakula vyote vya makopo na vilivyofungashwa kwenye makasha kwa siku 3; kwa sababu huko ndiko chanzo kikubwa cha BPA.

Kwahiyo ‘chakwanza’

Epuka/punguza vyakula vilivyofungwashwa kwenye mapaketi, tumia vyakula fresh.

Hata vyakula fresh kama samaki wengi wanakuwa na kiwango kikubwa cha BPA kutokana na uchafuzi wa bahari na maziwa uliokithiri kwa sasa.

Wakati mwingine hawa samaki wanaweza wakawa na kiasi kikubwa cha BPA kuliko hata samaki wa kopo.

Mbali na chakula..

Madhara ya BPA

1.      Kuongeza uzito na kitambi kwa wanawake na wanaume katika umri wowote.

BPA shida yake kubwa ni kuwa inaleta madhara kama homoni ya estrogen mwilini.

Kukiwa na BPA nyingi kunakuwa na madhara yanayotokana na kuwepo kwa wingi wa strogen ambayo ni pamoja na kuhamasisha mafuta kutunzwa zaidi mwilini.

Hata kama BPA ikipita kwenye ini ikapunguzwa makali bado inaleta madhara kwa wanadamu.

2.      Inapunguza misuli kwa wanaume

3.      Inapunguza nguvu za kiume

BPA inaweza kupita kwenye placenta na kuingia kwa mtoto na pia inaweza kupita kuingia kwenye maziwa ya mama. Kwahiyo inaweza ikaleta madhara hata kwa watoto wadogo.

Ujumbe wangu:

Epuka/punguza vyakula vilivyofungashwa kwenye makasha au kusindikwa ongeza vyakula fresh. Epuka/punguza matumiziya samaki. Ikiwa utapenda kutumia samaki tumia wenye mapezi na magamba.

Phthalates

Hii ni aina ya plastiki inayosababisha uzito mkubwa na kitambi; chanzo chake ni vyakula vya wanyama kama nyama, maziwa ya wanyama (kama yamekamuliwa na mashine.. mambo ya wazungu huko), mayai ya kuku na nyama ya kuku yenyewe.

Kwenye maziwa phthalates inatokana na mashine zinazotumika kukamulia maziwa. Maziwa yaliyokamuliwa kwa mikono yana phthalates kidogo mara kumi zaidi.

Wazo la muhimu

Kwenye vyombo vya plastiki kuna vile ambavyo vimetengenezwa kuhimili joto kali na vingine hapana. Huwa wanaandika kabisa.

Maana..

Ukitumia plastiki kwa chakula cha moto inazifanya hizo kemikali za plastiki BPA na phthalates kutoka kwenye chombo na kuchanganyikana na chakula.

Mfano hatarishi

 • Kunywa chai au uji kwenye vikombe, bakuli au sahani za plastiki
 • Kufungia maharage yaliyochemshwa au chakula chochote cha moto kwenye vikaratasi vya plastiki
 • Kutunzia chakula cha moto kwenye vyombo vya plastiki ambavyo havitengenezwa kuhimili joto.
 • Usiweke vyombo vya plastiki kwenye microwave badala yake vioshe tu kawaida
 • Usitumie vyombo vya plastiki vikiwa vimekwaruzika au
 • Vyombo vya plastiki usiviache juani

Ni vema kuepuka tabia hizo zinamadhara makubwa kwenye afya na hapa kwenye uzito mkubwa na kitambi haikuachi salama.

Vyombo hivi vitumike tu kwa dharura isiwe tabia yako kuvitumia hasa kwa vyakula vya moto. badala yake tumia vyombo vya udongo au glasi.

Hizo mbili ni kemikali ambazo zinatolewa na plastiki zinazoathiri mfumo wa homoni na kupelekea mtu kuongezeka mafuta.

Lakini..

Kuna sumu nyingine nyingi ambazo zinatolewa na plastiki kwa matumizi mabaya kama hayo ambazo zinaleta madhara mengine ya kiafya ikiwemo saratani.

Polycyclic aromatic hydrocarbons (PAHs)

Hii ni sumu ambayo inapatikana kwenye moshi wa magari, sigara na nyama ya kuchoma. Kwenye nyama; nyama ya nguruwe ina PAHs nyingi zaidi kuliko ya ng’ombe.

Madhara ya PAHs

 1. Inasababisha saratani.

Kwa sababu ya uwepo wa sumu hii kwenye mapishi ya nyama, mwaka 2015, nyama iliwekwa kwenye kundi la vitu vinavyoweza kusababisha saratani na nyama ya kopo kwenye kundi hatari zaidi kwenye kusababisha saratani.

 • Inaongeza uzito kuanzia kwa watoto na watu  wazima.

Bahati njema..

..PAHs haiwezi kujazana kwenye mwili, mwili unaiondoa kabisa kwa masaa 20.

Hata hivyo..

.. ni vema kutojitia sumu kwa ulaji nyama mkubwa. Epuka matumizi ya nyama au kama ukila isiwe kila siku.

Nyama iliyochemshwa ni nzuri zaidi kuliko iliyochomwa, kubanikwa au kukaangwa.[4]

Nyama inakuwa haizalishi hizi kemikali kama isipopikwa kwenye moto mkali usiozidi 260F.

Vile vile..

Kama umepanda mbogamboga karibu na barabara zenye magari. Osha vizuri mbogamboga kwa maji tiriri ili kuondoa PAHs ambazo zinakuwa zimekaa kwenye mbogamboga kutokana na moshi wa magari.

Hapa Napata mashaka makubwa kwa wanaofanya mazoezi barabarani wanapishana na magari…

Ni kupoteza muda

.. Kufanya mazoezi ya aerobic kama kukimbia barabarani kwenye magari mengi unajiumiza.

Unavuta PAHs nyingi sana. Fanya mazoezi sehemu yenye hewa safi. Ili uvute hewa safi itakayokusaidia kupata faida za mazoezi.

Kuna mengi ambayo bado hayajafahamika kuhusu jinsi uchafuzi wa mazingira na kemikali vinavyosababisha uzito mkubwa na kitambi na kuletea athari kwenye afya ya binadamu kwa ujumla.

Hata hivyo ni vizuri kujikinga kwa elimu kidogo iliyopo kwa kuchagua kula zaidi vyakula vinavyotokana na mimea.

NA

Chukua tahadhari nilizoelekeza unapotumia vyombo vya plastiki kutunzia, kubebea au kulia chakula.

5 1 vote
Article Rating
Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Asheri
Asheri
29 May 2023 13:29

Dr Nature huduma yako imetukuka sana. Imenisaidia kutoka kwenye matatizo ambayo ingenigharimu mamilioni. Mungu akubariki sana doctor wangu ❤️

Share
Scroll to Top